Kwa mujibu wa Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Jumuiya ya Kitaifa ya Kiislamu ya Al-Wifaq ya Bahrain, katika taarifa yake, imetaka kupitiwa makubaliano ya kijeshi na kiusalama kati ya Ufalme wa Bahrain na tawala za kigeni, pamoja na kufanyika mageuzi ya kisiasa ambayo imeyaita “ya msingi”; mageuzi yenye lengo la kuimarisha nafasi ya matakwa ya wananchi katika kuendesha mambo ya nchi.
Jumuiya hiyo ya Bahrain imesema katika taarifa hiyo: Nchi hii iko katika hatua nyeti ya kikanda. Utegemezi wa nchi kwa makubaliano na mifumo ya kijeshi na kiusalama, sambamba na kuwa mwenyeji wa vituo na vikosi vya kigeni, unazua maswali kuhusu kiwango cha mamlaka ya kitaifa na uwezo wa nchi kujitenga na migogoro na vita vinavyoendelea katika eneo hilo.
Jumuiya ya Al-Wifaq imesisitiza umuhimu wa kuiweka ardhi, maji ya bahari na anga ya Bahrain katika hali ya kutokuwa na upande dhidi ya hatua yoyote ya kijeshi inayoilenga nchi nyingine.
Jumuiya hiyo imetaka kupitiwa makubaliano yaliyopo ya kijeshi na kiusalama na kuandaliwa mtazamo wa kitaifa kuhusu usalama na ulinzi ambao, kwa mujibu wa taarifa hiyo, uzingatie maslahi, mamlaka na uwezo wa Bahrain, na kuzuia ardhi ya nchi hiyo isigeuzwe kuwa uwanja au kituo cha kuanzisha migogoro ya kikanda.
Katika muktadha huo, Jumuiya ya Kiislamu ya Al-Wifaq ya Bahrain imekosoa kuendelea uhusiano rasmi na utawala wa Israel, na hasa makubaliano ya kuhalalisha uhusiano na utawala wa Kizayuni, na kusema: Kuendelea kwa uhusiano huu hakuendani na msimamo wa wananchi wa Bahrain kuhusu vita vya Ghaza na Lebanon, wala na kile ambacho jumuiya hiyo inakiita “sera za Israel dhidi ya ardhi za Palestina na Kiarabu.”
Jumuiya ya Kiislamu ya Al-Wifaq imetaka makubaliano ya kuhalalisha uhusiano yakomeshwe na kufanyika mapitio ya aina mbalimbali za uwepo wa Israel nchini Bahrain, ikiwemo uwepo wa kidiplomasia, kiusalama, kijeshi, kiutamaduni na kibiashara. Wakati huo huo, imetaka kuanzishwa kwa uhusiano wa kikanda unaozingatia kuheshimiana, ushirikiano na maslahi ya pamoja.
Katika uwanja wa siasa za ndani, jumuiya hiyo imetaka kufanyika mabadiliko ya kisiasa ya msingi kwa kuzingatia kanuni kwamba “wananchi ndio chanzo cha mamlaka zote.”
Jumuiya hiyo ya Kiislamu imeyataja mageuzi ya kisiasa kuwa miongoni mwa madai yanayohusiana na historia ya harakati za kitaifa nchini Bahrain, na imesisitiza: Kujibu matarajio na matumaini ya wananchi kunahitaji kuimarishwa kwa ushiriki wa wananchi katika kufanya maamuzi.
Taarifa hiyo pia imezungumzia hali ya kiusalama na kisheria ya ndani, na imetaka kuachiliwa wanazuoni wa dini na wafungwa, pamoja na kusitishwa kile ilichokiita “kampeni ya kiusalama dhidi ya raia wa Kishia.” Jumuiya hiyo inaamini kwamba kushughulikia hali ya mvutano wa ndani kunahitajia hatua za kisiasa na kisheria zitakazosaidia kujenga upya imani na kuimarisha amani ya kijamii.
Jumuiya ya Kiislamu ya Al-Wifaq pia imesisitiza haki ya wananchi kutumia haki zao za kisiasa na kueleza utambulisho wao wa kitaifa na kidini, na imesisitiza umuhimu wa kuheshimu utambulisho wa Kiarabu na Kiislamu wa Bahrain na kukataa kile ilichokiita “jaribio la kutilia shaka uaminifu wa wananchi kwa nchi yao kwa msingi wa misimamo yao ya kisiasa au kidini.”
Jumuiya ya Al-Wifaq ilihitimisha taarifa yake kwa kuwasalimia wananchi na kupongeza kile ilichokiita “subira na nidhamu katika kukabiliana na kampeni za uzalendo hasi, uchochezi na kauli za kimadhehebu,” na kusisitiza kushikamana kwake na kile ilichokiita “misingi ya kitaifa inayohusiana na utambulisho na historia ya Bahrain.”
Maoni yako